Maafisa wa utawala katika Tarafa ya Kabazi, Kaunti Ndogo ya Subukia wamewatahadharisha wakazi katika eneo hilo wanaowaficha walemavu kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakizungumza siku ya Alhamisi kwenye hafla ya kuwasajili walemavi katika Tarafa ya Kabazi kwenye Hospitali ya Kabazi, Maafisa hao walisema kuwa baadhi ya familia huona aibu kufuatia hali ya wapendwa wao kuwa na changamoto za kimaumbile na kuwaficha kwa kuwafungia ndani ya nyumba wasionekane au tambulike.

“Walemavu wana haki kama mmoja wetu asiye na ulemavu. Hivyo basi kila mtu anastahili kuziheshimu haki hizo na familia zinazo waficha walemavu hao wajue kwamba mkono wa sheria utapatana nao,” alisema Paul Rong’e Naibu Chifu wa Kata ndogo ya Kabazi.

Zaidi ya walemavu 80 kutoka maeneo ya Rugongo, Kabazi, Gitura, na Munanda walijitokeza kusajiliwa kwenye zoezi hilo la siku ya Alhamisi.

Inakisiwa kuwa baadhi ya walemavu walishindwa kufika katika eneo ili wasajiliwe katika shughuli hiyo iliyo shirikisha ukaguzi wa kimatibabu 

“Tulitarajia idadi ya walemavu kuwa kubwa, tarajio ambalo halijahitimizwa. Huenda wengi walishindwa kufika hapa, lakini tutazuru vijijini ili kuwatambua wengine ambao hawakusaliwa leo,” alisema Rong’e.

Aidha baadhi ya waliodai kuwa na ulemavu hawakusajiliwa baada ya ukaguzi wa kimatibabu kubaini ulemavu wao unatokana na kutopata matibabu na hali inaweza badilishwa au rekebishwa kupitia kupata matibabu.

Serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti ya Nakuru inalenga kuwasajili na kuwatambua walemavu wote katika Kaunti ili waweze kuwezeshwa kwa kupewa msaada.