Wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Pwani wamepongeza uzinduzi wa kituo cha kwanza katika eneo la Pwani, cha kutibu ugonjwa wa kisukari.
Kituo hicho kilidhaminiwa na shirika la Novo Nordisk la Denmark likishirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Ijumaa, wagonjwa hao wakiongozwa na Jamali Mohamed walisema kuwa kituo hicho kitasaidia wengi ikilinganishwa na hapo awali ambapo wagonjwa wengi walitaabika sana.
Aidha, wameitaka serikali ya kaunti kutoweka ada ya juu ya kutibu maradhi hayo ya kisukari kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya gharama ya juu.
Shirika la Novo Nordisk linalenga kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa huo, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kuhakikisha watu wanapimwa kujua iwapo wanaugua ugonjwa huo.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Joho, alisema kuwa atahakikisha watu wanaougua ugonjwa huo wa kisukari wanapata matibabu bora katika hospitali zote za Kaunti ya Mombasa na kusisitiza kuwa atashirikiana na wadau mbali mbali kuboresha sekta ya afya.