Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa umewashinikiza wanafunzi kusalia majumbani mwao hadi pale mgogoro uliyopo kwa sasa katika chuo hicho utakapotatuliwa.

Kulingana na Naibu Rais wa Muungano huo Oseko Denis, hatua ya wasimamizi wakuu wa chuo hicho kuwataka wanafunzi kurejea chuoni humo na Sh2,650 kila mwanafunzi za kugharamia uharibifu uliotekelezwa wakati wanafunzi hao waliogoma.

Akiongea na wanahabari nje ya chuo hicho mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Oseko alisema kwamba wamemuandikia barua Waziri wa Elimu nchini Profesa Jacob Kaimenyi kuingilia kati mgogoro wa chuo hicho na kutatua masaibu yanayowakumba wanafunzi hao.

"Tumemuandikia barua Profesa Jacob Kaimenyi kuingilia kati mgogoro huu na kuhakikisha kwamba haki inapatika kwa sababu wasimamizi wa chuo hichi wanatumia mamlaka yao kutudhulumu sisi wanafunzi,” alisema Oseko.

Oseko alisema kwamba wanafunzi hawana shida na Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Josephat Mwatela, huku akidai kuwa kamati ya usimamizi wa chuo hicho ndiyo inayongoza chuo hicho ili kujibinafsisha kutoka kwa mifuko ya wazazi.

"Sisi hatuna shida na Naibu Chansela wetu lakini lazima ajadiliana nasi kwa niaba ya wafunzi wa chuo hiki na kuondoa viwango vya pesa walivyoweka kama gharama ya kulipa harasa wanayosema tulisababisha wakati wa mgomo,” aliongeza Oseko.

Wakati uo huo Katibu wa muungano huo Hillary Nyang’or alisema kwamba kamwe wanafunzi hawatarudi chuoni na wala hawatalipa gharama hiyo huku akisema kwamba wanachohitaji kwa sasa ni vikao vya mazungumzo na wasimamizi wa chuo hicho ili kujadili masaibu yanaowakumba wanafunzi hao.