Wakaazi wa eneo la Subukia Valley katika Wadi ya Subukia wamepata afueni baada ya Serikali ya Kaunti ya Nakuru kusikia kilio chao cha kuwakarabatia barabara pamoja na bwawa lililoko katika eneo hilo.
Wakiongozwa na Njire Muhia, wakaazi hao walisema kuwa kwa muda wamekuwa wakiteseka kufuatia ubofu wa barabara hilo ulio sababishwa na mvua kubwa iliyo shuhudiwa katika eneo hilo msimu uliopita na pia kuacha mabwawa ya maji ambayo yamekuwa tegemeo lao la maji kwa miongo mingi kujaa mchanga na kuvunja kingo zake.
Tayari mwanakandarasi anaye karabati barabara hizo ameanza kazi na Mwakilishi wa Wadi hiyo katika Bunge la Kaunti ya Nakuru Peter Njoroge Muchiri amehakikisha kwamba kazi hiyo inatarajiwa kukamilika kwa majuma kadhaa yajayo.
“Ninatoa msukumo kwa Serikali yetu ya Kaunti kuona fedha nyingi zinatengewa miradi katika Wadi yangu hasa ikizingatiwa kuwa ni kitovu cha Kilimo cha nyanya na viazi,” alisema Muchiri.
Naye mkaazi mwingine anayejulikana kama Muhia alisema wamekuwa wakiteseka kufuatia baadhi ya daraja kusombwa na maji na licha ya juhudi zao za kutafuta mbinu mbadala za kujenga vivukio hali bado haikuimarika.
Mwenzake Peter Karugu alisema, “Ingawa sisi kama wakazi wa Subukia Valley tunashukuru Serikali ya Kaunti kwa hatua hii, hatujaelewa ni kwa nini imekawia kusikia kilio chetu. Ubovu wa barabara hizi umelemaza usafirishaji wa bidhaa za kilimo kutoka mashambani mwetu.”
Hata hivyo, Mwakilishi Muchiri alisema mvua kubwa inayo shuhudiwa kwa sasa katika eneo hilo pamoja na ucheleweshaji wa utoaji wa fedha umesababisha ukarabati huo kufanywa kwa njia ya upole.