Seneta wa Kaunti ya Nyamira Mong’are Okong’o amewaomba Machifu wa Kaunti hiyo kuhakikisha kuwa watoto wanaenda shule.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumamosi katika Shule ya Msingi ya Gekonde ilioko eneo Bunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Nyamira, Seneta Mong’are alisema watoto wengi hufanyishwa kazi na wazazi wao na kutoenda shule jambo ambalo amegadhabishwa nalo.

Wakati uo huo, Seneta huyo alikiri kuwa watoto hufanya kazi ya kusomba matofali, wengi wao wakitoka katika eneo Bunge la Kitutu Masaba na Mugirango Kaskazini.

“Watoto wengi hawaendi shule na kuafanya kazi za nyumbani. Nawaomba Machifu wa Kaunti hii ya Nyamira nzima kuhakikisha kuwa watoto wote kutoka vijijini wanaenda shule,” alisema Seneta Mong’are.  

Aidha, Seneta huyo alisema anahitaji viwango vya masomo katika Kaunti ya Nyamira kuinuka zaidi baada ya walimu kutia motisha wanapowafundisha wanafunzi.

“Nitashirikiana na wakazi wa Nyamira kuona viwango vya elimu vimenawiri zaidi katika Kaunti yetu ili watoto wetu waje kuwa viongonzi wa kesho,” aliongezea Senator Mong’are.

Kwa upande mwingine, wakaazi wa Kaunti ya Nyamira walimpongeza Seneta wao kwa ahadi anazozitoa haswa katika sekta ya elimu na kutimiza.

“Tunamwomba Seneta wetu atimize kwa haraka yale tunahitaji katika Kaunti yetu ili ijulikane kwa kimasomo,” alihoji Zachary Osiemo mkaazi wa Nyamira.

Seneta Mong’are alisema kuwa wakaazi wa Nyamira wanahitaji kupanda miti ili kuongeza idadi ya miti kutoka asilimia 35 hadi 45 katika Kaunti ya Nyamira.