Serikali imeulizwa kuwapiga marufuku baadhi ya wanakandarasi ambao wanakiuka sheria na kufanya kazi duni licha ya kiasi kikubwa cha pesa za umma kuwekezwa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wito huu umetolewa na wakazi wa mtaa wa Tayari wilayani Molo ambao walimfurusha mwanakandarasi mmoja kwa madai ya utendakazi hafifu pamoja na kukosa uzoefu wa kutekeleza ukarabati wa barabara.

Joseph Njihia kwa niaba ya wakaazi hao waliojawa na ghadhabu amesema licha ya wenyeji kulalamikia hali mbaya ya barabara hiyo, serikali ilituma mjenzi ambaye anakiuka maadili pamoja na sheria za utendakazi wa miradi ya umma.

Amesema wananchi hawatavulimilia kazi mbovu kufanywa kwa ufadhili wa fedha za umma akiuliza serikali kuwatuma wahandisi wake ili kutadhimini mradi huo ambao unajengwa vibaya.

Aidha wananchi hao wamesema iwapo mradi huo utakamilika jinsi ulivyo ,huenda eneo hilo la barabara ya Molo- Mau Summit likawa hatari haswa kwa madereva wa malori yenye uzani mkubwa.

Wakati huo huo wakazi hao wameitaka serikali kushinikiza wanakandarasi kuwapa vijana nafasi za kazi huku wakidai kwamba baadhi ya wanakandarasi huleta vijana kutoka maeneo mengine.

Wamesema baadhi ya kazi  za ujenzi hazihitaji ujuzi mkubwa wakisema kila mradi wa maendeleo ni sharti unufaishe wakaazi  kikamilifu.