Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mke wa gavana wa Nakuru Lucia Kinuthia amesema kuwa watu wengi wanafahamu kuhusiana na saratani ya matiti lakini hawachukui hatua za kubaini iwapo wana ugonjwa huo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mwezi wa kujifahamisha kuhusiana na ugonjwa huo wa saratani katika gereza la GK lililo kwenye wadi ya London, katika eneo bunge la Nakuru Magharibi, Bi Kinuthia alisema ingawa watu wengi wanafahamu kuhusiana na saratani ya matiti, sio wengi walio na mpango utakaowapelekea kubaini maradhi hayo yakiwa katika hatua za mwanzo mwanzo za ugonjwa huo.

Hata hivyo, amepongeza Sekta ya afya kwenye kaunti ya Nakuru kwa kujibidiisha kutoa elimu kuhusiana na maswala ya saratani na pia kwa kuanzisha harakati za kufanya uchunguzi wa kubaini iwapo mtu ana ugonjwa huo kwenye vituo vya kiafya.

Kando na hayo, alitoa sodo pamoja na vyakula mbalimbali kwa wanawake walio katika gereza hilo la wanawake.

Baadhi ya huduma zilizoendelezwa katika kuzindua mwezi huu ni kama vile kutoa elimu kuhusiana na upangaji uzazi na uchunguzi wa kubaini iwapo mtu ana saratani miogoni mwa huduma zingine.

Bi Kinuthia alikuwa ameandamana na Waziri wa afya kwenye kaunti ya Nakuru Dkt Mungai Kabii na afisa mkuu wa afya ya uma kwenye kaunti Dkt Samwel Mwaura miongoni mwa maafisa wengine kwenye kaunti ya Nakuru.

Oktoba ni mwezi wa kujifahamisha kuhusiana na ugonjwa wa saratani na hutumika kama kampeni ya kila mwaka ya kuongeza elimu kuhusiana na ugonjwa huo.

Katika kuadhimisha mwezi huu, Kaunti ya Nakuru kupitia kwa kitengo chake cha afya itakuwa ikiendeleza uchunguzi wa kubaini iwapo mtu ana ugonjwa huo kwenye kaunti ndogo za Nakuru.