Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewaonya mawaziri wake wanaozembea kutekeleza miradi mbalimbali iliyoko chini ya wizara zao.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye mkutano wa faragha na spika wa kaunti hiyo Joash Nyamoko, Kiongozi wa walio wengi Laban Masira, na kiongozi wa wachache Jackson Mogusu, gavana Nyagarama aliagiza utekelezaji wa miradi iliyokwama kwa kuwa tayari bunge la kaunti hiyo lilikuwa limetenga pesa za kufadhili miradi hiyo.

Aliongeza kusema kuwa baadhi ya mawaziri wanaendelea kuwasilisha ripoti tofauti na zile wanazo wasilisha wawakilishi wa wadi.

"Sitaki kupuuza wanayoyasema wawakilishi hawa wa wadi kwa kuwa kwa mara nyingi wao ndio wanaotangamana na wananchi, na sasa lalama zinawaendea mawaziri wangu ambao nawaonya kuimarisha utendakazi wao ili waafikie matakwa ya wananchi." alisema Nyagarama.

Gavana Nyagarama aliongeza kwa kutishia kuwafuta kazi mawaziri ambao hawataimarisha utendakazi wao.

"Sharti mawaziri wawe tayari kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoko chini ya wizara zao, na iwapo hawapo tayari kufanya hivyo, nawaomba wajiuzulu mapema au nichukue hatua ya kuwafuta kazi kwa kuwa nahitaji kuona pesa za umma zikitumika vizuri." alionya Nyagarama.

Akiunga mkono usemi wa gavana Nyagarama, kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira alisema kuwa mawaziri wanafaa kuitembelea na kuikagua miradi mbalimbali iliyoko chini ya wizara zao.

"Kama mkuu wa idara inafaa utembelee na kuikagua miradi iliyoko chini ya wizara yako, lakini iwapo huwezi kufanya jambo dogo kama hilo yafaa gavana akufute kazi," alisema Nyagarama.

Haya yanajiri siku chache zilizopita baada ya bunge la kaunti hiyo kushtumu serikali ya kaunti hiyo kwa kujikokota kutekeleza miradi muhimu.