Mkuu wa wizara ya uchukuzi na miundomsingi John Mosonik amemtaka kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kukoma kuingilia maswala ya shirika hilo.
Mosonik amesema kuwa yeye ndiye mkuu wa idara hiyo na sharti viongozi wengine wakome kuweka siasa katika suala hilo, huku akiongezea kuwa tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mamlaka na usimamizi mzima wa shirika hilo unafanyiwa uchunguzi ili kubaini ni nini hasa kiliweza kusababisha zogo la hivi majuzi ambako watu waliweza kukanyagana.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika kivuko hicho cha Likoni kwenye ziara rasmi ya kukagua moja kwa moja, Mosonik alisema kuwa kamishna wa kaunti sharti aheshimu wizara hiyo, na kusema kama kuna ushahidi wowote kuwa shirika hilo linajihusisha na ufisadi baadaye ukweli utatoka baada ya kuanzishwa uchunguzi kuhusiana na suala hilo.
“Hiki ni kitengo changu, na serikali ina njia ya kukabili masuala yake, hivyo viongozi badala ya kuanza kutiana lawama ni vyema kutoa njia na kutafuta mwafaka wanapoona shida mahali, na serikali ipo tayari kuanza kuchunguza kilichojiri,” alisema Mosonik.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatatu wakati kulitokea msongamano kwenye kivuko hicho, kamisha wa Kaunti Nelson Marwa alimshtumu mkurugenzi mkuu wa shirika la feri Hassan Musa kwa kutumiwa vibaya na baadhi ya watu na kutoa huduma zisizoridhisha kwa umma na wateja wao.