Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Msimamizi wa maswala ya teknolojia katika tume ya mgao wa mapato nchini CRA, amesema serikali ya Kaunti ya Nyamira inaendelea kupoteza pesa nyingi kupitia ukusanyaji wa ushuru.

Hii ni baada ya kubainika kuwa serikali ya kaunti hiyo inakusanya ushuru ikitumia mradi wa awali, badala ya kutumia teknolojia ya kisasa, jambo linalopelekea serikali hiyo kuendelea kupata hasara na kupoteza pesa nyingi.

Akizungumza siku ya Jumatano katika kikao kilichowajumuisha wawakilishi wadi katika mkahawa mmoja mjini Nyamira, Joseph Kuria alisema ukosefu wa kutumia teknolojia ya kisasa ndio umechangia serikali ya kaunti hiyo kuendelea kupata hasara kubwa.

“Kaunti nyingi hapa nchini zimeanza kukusanya ushuru kwa njia ya teknolojia ya kisasa. Naomba kaunti ya Nyamira kuweza kukumbatia mradi huo wa teknolojia ya kisasa na kuanza kukusanya ushuru wao kwa njia hiyo ili kuzuia hasara,” alisema Kuria.

Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Nyamira inapaswa kununua mashine hiyo ya kukusanya ushuru kwa njia ya teknologia.

Hii ni baada ya bunge la kaunti hiyo kupitisha mswada wa kununua mashine ya kukusanya ushuru lakini hilo bado halijashughulikiwa kikamilifu.

“Shida tuliyonayo katika ukusanyaji ushuru hapa Nyamira ni kuwa mtendaji hajaweka mipangilio kamili ya kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinashughulikiwa kwa kununua mashine hiyo,” alisema Nyamoko.