Seneta wa Kaunti ya Nakuru James Mungai amesema wananchi hususan wakazi wa Kaunti ya Nakuru, wanafaa kujilaumu kutokana na madai ya ufisadi yaliyoripotiwa katika kaunti hiyo hivi majuzi.
Akizungumza na mwandishi huyu kwa njia ya simu siku ya Jumatano, Seneta Mungai alisema kwamba wananchi hawakuwapiga msasa kikamilifu viongozi walio mamlakani kwa wakati huu, wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka wa 2013.
Hii ni kutokana na ripoti iliyotolewa na mkaguzi mkuu wa pesa za serikali Edward Ouko ya matumizi ya kifedha ya mwaka wa 2013 hadi 2014.
Seneta Mungai alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa viongozi waliotwikwa jukumu la kusimamia raslimali ya mwananchi wa kawaida ndio wanaopora pesa za mwananchi asiyekuwa na ufahamu wala hatia yoyote.
Aidha alisikitika kuwa kati ya shilingi bilioni saba zilizotengewa Kaunti ya Nakuru, ni shilingi milioni mia nane tu ndizo zilizotumika katika miradi ya maendeleo.
“Wakazi hawapaswi kunyamaza bali wanafaa wajibidiishe kujua mambo yanavyoendelea katika Kaunti ya Nakuru,” alisema Mungai.
Isitoshe, ameelezea hofu yake kutokana na ripoti ya hesabu itakayotolewa ya matumizi ya kifedha ya mwaka wa 2014 hadi 2015, akidai kuwa pesa zaidi huenda zikawa zimefujwa.
Hata hivyo, seneta huyo ametoa wito kwa wananchi wa Kaunti ya Nakuru na pia kwa nchi nzima kwa ujumla, kuwa makini na kuwachagua viongozi wenye maadili na uwazi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.