Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya madai kuwa vijana wa kuweka usalama mitaani almaarufu ‘Community policing’ kutaka serikali kuwatambua kwa kuwalipa, mwenyekiti wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi amewataka wahusika kuhudumia nchi yao na kuwa serikali haina hela za kuwalipa.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa sharti kila mmoja awajibike kwa kutoa usalama katika nchi yake, na vijana wanafaa kujihusisha katika kutoa usalama katika mitaa wanayokaa, ili kuonyesha uzalendo kwa nchi yao.

Akiongea siku ya Jumanne mjini Mombasa katika hafla ya kujadili masuala ya usalama, Kaguthi aliwataka wakazi kusaidiana na kuipatia serikali nafasi nyepesi ya kutekeleza masuala ya usalama, badala ya kusubiria idara za usalama kuwatekelezea kila kitu.

Mwenyekiti huyo aliwasihi wakazi wa Kaunti ya Mombasa kukumbatia mwito wa nyumba kumi ili kuweza kutoa habari kuhusiana na wale wakazi ambao wanawatilia shaka kwenye maeneo wanamokaa ili kupunguza visa vya uhalifu miongoni mwa jamii.

“Jukumu la usalama linaanza na sisi, hivyo basin ni vizuri zaidi kuweka usalama pale mahali tunakaa huku serikali nayo ikijitahidi kutoa huduma za usalama, na wale wanataka kulipwa ndio watoe usalama kwenye jamii nawaomba kama wazalendo wa nchi hii kufanya kazi hiyo kwa kujitolea kwa sababu hii ni nchi yetu,” alisema Kaguthi.