Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyibiashara wanaoendeleza shughuli zao katika maeneo yaliyokaribu na benki mjini Kisii, huenda wakafurushwa kufuatia visa vya wizi katika benki vinanyotekelezwa na majambazi katika miji mikuu.

Akiongea katika Uwanja wa Gusii siku ya Jumatano, mwenyekiti wa muungano wa benki mjini Kisii, Samwel Nyaundi, ameiomba idara ya usalama kwa ushirikiano na uongozi wa kaunti hiyo, kuhakikisha kuwa wafanyibiashara wadogo wanaouza bidhaa zao karibu na benki mjini humo, wamepelekwa sehemu zingine kama njia moja ya kuimarisha uslama.

“Shughuli hiyo inapaswa kufanywa kwa utaratibu bila uharibifu wowote wa mali ya wafanyibiashara hao,” alisema Nyaundi.

Akizungumzia swala hilo, Naibu gavana wa Kaunti ya Kisii, Joash Maangi, alisema kuna umuhimu wa kuimarisha usalama katika benki.

Maangi alitoa ahadi kuwa serikali ya kaunti hiyo itahakikisha kuwa shughuli hiyo imefanywa kwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria.