Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nakuru Mary Mbugua, amesema anaunga mkono hatua ya aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Anne waiguru kujiuzulu kutoka wadhifa wake.
Akizungumza siku ya Jumapili baada ya ibaada katika Kanisa la PCEA Shabaab mjini Nakuru, Mbugua alisema kuwa ingawa anaunga mkono kujiuzulu kwa Waziri Waiguru, Wakenya watakosa huduma zake serikalini.
“Mimi nilisikitika sana kama mama baada ya Waziri Waiguru kujiuzulu kwa sababu nilijua kwamba vijana wa taifa hili watakosa huduma zake sana. Hata hivyo, Waiguru amedumisha heshima yake na heshima ya kina mama nchini kwa hatua aliyochukua,” alisema Mbugua.
Mbugua aidha alimlaumu katibu mkuu katika Wizara ya Ugatuzi na Mipango Peter Mangiti kwa masaibu yaliyomkumba Waiguru.
Mbugua alisema kuwa Mangiti anafaa kukabiliwa kwa mujibu wa sheria, ili haki ipatikane, kufuatia kupotea kwa takribani shilingi milioni mia saba tisini na moja huku za shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS.
“Mangiti anajua yaliyotokea katika sakata hii ya NYS na amemsababishia Waiguru masaibu mengi sana hadi akajiuzulu. Anapaswa kukabiliwa na sheria na aelezee kile anajua kuhusu wizi huo,” alisema Mbugua.