Kaunti ya Mombasa imezindua utaratibu na mfumo maalum wa kufuatwa kuweza kuratibu jiji la Mombasa kwenye mpangalio wa majengo na miundomsingi kwa jumla kwa ushirikiano na serikali ya Japan, JICA.
Utaratibu huo ambao ulipewa jina 'Gate City Master Plan', unalenga kutoa suluhu la matatizo ya uwepo wa majengo ambayo yamejengwa vibaya, na kuwa na miundomsingi hasa ile ya mabomba ya maji taka ambayo ni yenye viwango vya chini.
Akiwahutubia maafisa wa serikali ya Kaunti, umma na pamoja na vyombo vya habari siku ya Jumatano kwenye hafla ya uzinduzi rasmi mjini Mombasa, Naibu wa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hezel Katana alisema kuwa Kaunti ya Mombasa inalenga kuwa miongoni mwa miji iliyo na miundomsingi bora na imara zaidi kote ulimwenguni kupitia kwenye mradi huo.
Bi Katana alisema kuwa Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa kaunti na miji ambayo kufika karne hii imeweza kutambulika kote duniani kwa kuwa na majengo ya kuvutia na hali imechangia kuweza kuwaleta watalii kila mwaka na mradi kama huo utaliboresha jiji hilo zaidi.
Naibu huyo gavana aliongeza kusema kuwa mbali na kuweka mazingira mazuri kwa wakazi pamoja na wageni, mradi huo utaweza kupunguza visa vya misongamano wa watu ambao wanakaa kwenye nyumba duni, misongamano ya magari ambayo husababishwa na barabara mbovu pamoja na kuleta suluhu katika utapakaji wa taka katika mji.