Zaidi ya Sh4.2m zimetumiwa kuwanufaisha vijana ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Akizungumza na wanahabari mjini Nakuru siku ya Jumanne, mkurugenzi wa Hazina ya Kutengeneza Filamu ya Afrika Mashariki, Mudamba Mudamba amedhibitisha kwamba hazina hiyo maarufu kama Docubox imetoa pesa hizo kwa vikundi 18 kutoka Nairobi pamoja na Kaunti ya Nakuru.
Mudamba alisema kuwa lengo la hazina hiyo ni kuwawezesha vijana kutumia filamu kuelezea matukio mbalimbali, huku kila kikundi kinachofaulu kikipewa zaidi ya Sh200,000.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo itawawezesha vijana kutengeneza filamu zao wenyewe, sawa na kubuni ajira kwa vijana humu nchini.
Mudamba ambaye alikuwa ameandamana na mmoja wa watengenezaji filamu kutoka nchini Norway Mkurugenzi Anders Somme Hammer, alisema kwamba pesa hizo hazitozwi riba yoyote na hivyo basi vijana wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira humu nchini, wataweza kujiendeleza.
Ingawa kwa sasa wanafanya kazi humu nchini katika Kaunti ya Nairobi, Machakos pamoja na kaunti ya Nakuru, ameweka wazi kwamba wanalenga kusambaza huduma zao nchini Uganda pamoja na Tanzania.
Tangu kuanzishwa kwa hazina hiyo ya kutengeneza filamu, February 2013 kwa ufadhili wa wakfu wa Ford, Mudamba ametoa wito kwa jinsia ya kike kujitokeza pia, ili waweze kutumia fursa hiyo na kuunda filamu zao.