Baada ya mashambulizi ya wakazi pamoja na kuuliwa kwa afisa wa usalama hivi majuzi katika mji wa Old town mjini Mombasa, wakazi sasa wamehakikishiwa kuwa usalama wao utaangaliwa na kuombwa kusaidia serikali na idara ya polisi kuweka usama kwa kuripoti visa vya ukosefu wa usalama katika mji huo.
Akiongea na waandishi wa habari katika mji wa Mombasa, kamanda wa polisi, Francis Wanjohi alisema kuwa usalama wa kila mwananchi na mkazi wa eneo la kaunti ya Mombasa utaangaliwa, na kuonya vijana mbao wamekuwa wakijihusisha na masuala ya uhalifu ambapo aliwataka wazazi kuwajibikia masuala ya wanao kwa kuwaelekeza kwa sababu wengi wa wahalifu ni vijana ambao hawana kazi.
Kamanda huyo alisema kuwa wakazi sharti washikakane mikono dhidi ya kupigana na masuala ya ukora na uhalifu ambao umeanza kukithiri katika mji huo.
Siku ya Jumatano wiki jana, wakazi walikuwa wametoa lawama kwenye idara la polisi kwa kuzembea kazini kufuatia wakazi kushambuliwa wiki jana ambapo baadhi ya wakazi ambao walikongamana katika uga wa umma wa Makadara kuadhimisha siku kuu ya Eid waliweza kupigwa na kuibiwa na zaidi ya vijana kumi ambao walikuwa wamejihami na marungu na panga.
Kisa kingine kilitokea siku tatu zilizopita baada ya polisi kupigwa na watu wasiojulikana na kunyanganywa bundiki ambapo, wakazi walitoa lawama kwa idara husika za usalama, na kuiomba serikali kuu kuongeza maafisa wa polisi wa kupiga doria kwenye maeneo mengi kwenye kisiwa hicho cha Mombasa.