Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Askari wanaohudumu kwenye kivuko cha feri huko Likoni Mombasa waliponea kichapo kutoka kwa umati siku ya Ijumaa usiku baada ya kisa ambacho wahudumu hao walihusika kumudhulumu mama mmoja kwa madai kuwa aliingia kwenye banda la wanaume badala ya la wanawake la kungojea feri.

Kulingana na Cyrus Juma ambaye alishuhudia kisa hicho, askari hao walimbeba mwanamke huyo juu kwa juu na hata kupururwa chini alipoonekana kukaidi amri yao.

Juma alisema kuwa walikasirishwa na jinsi waweka usalama hao walimshika mama huyo hata kuweka uchi wake wazi, jambo lililowagadhabisha watu walikuwa wanaingia kwenye eneo la kuongojea feri, ndiposa wakaanza hatua ya kuwakabili 'masoja' hao ambao walionekana kuwa na kiburi hata kuanza kuwafukuza wakazi hao.

“Mimi sijawahi kushuhudia mama akishikwa hivi kama gunia la mboga, hawa watu hawana utu, kwani wana haki gani ya kumshika huyo mama hivyo, si mna wanawake ambao wanaingia kwenye banda la wanaumme na kuchanganyikana, huu si udume kuwili, wanajifanya kutetea umma ilhali wameshindwa kazi,” alisema Juma.

Hata hivyo, shinikizo za umma ziliwafanya askari hao kumwachilia mama huyo na juhudi za kutaka kuongea na wahudumu hao hazikufua dafu kwani walidai kuwa hawakuwa tayari kuongea na wanahabari.