Wakaazi wa kaunti ya Nyamira wamehimizwa kutembelea vituo vya afya ili kupimwa na kujua iwapo wameathirika na aina mbalimbali za saratani.
Akihutubia katika eneo la Nyansabakwa, gavana John Nyagarama alisema kuwa asilimia kubwa ya wakaazi wa kaunti hiyo hawana ufahamu iwapo wameathirika na aina mbalimbali za saratani, hali inayo hatarisha maisha yao.
"Wakaazi wengi wa kaunti hii hawana ufahamu iwapo wameathirika na aina mbalimbali za ugonjwa wa saratani na hilo ni swala ambalo linaweza hatarisha maisha yao kwa kuwa idadi nyingi huanza kutibu saratani wakati ambapo imefika katika hali ya hatari, hali inayofanya kuwa vigumu kwa saratani hizo kuthibitiwa," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha amewahimiza akina mama wajawazito kujifungulia hospitalini ili waweze kuangaliwa kwa makini na wahudumu wa afya akisisitiza umuhimu wa masomo kwa kuwahimiza wazazi kuwapeleka wanao shuleni ili waweze kupata masomo yatakayo wafaa siku zao za usoni.
"Ni jambo zuri kusikia kwamba akina mama wamejifungua vizuri ila ombi langu kwao ni kuhakikisha kuwa wanaenda hospitalini kwa kuwa watahakikishiwa huduma bora na wahudumu wa afya na iwapo kutatokea jambo la dharura, itakuwa rahisi kina mama hao kushughulikiwa," aliongezea Nyagarama.