Share news tips with us here at Hivisasa

Majumba mengi kisiwani Mombasa yamejengwa barabarani na kupuuza mpangilio wa ramani ya jiji.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, Naibu Gavana wa Mombasa Hazel Katana alisema tatizo kuu kwa sasa ni kuwa nyumba hizo zimejengwa kiholela bila idhini ya maafisa wa upingaji wa ramani ya jiji, hivyo basi kukiuka sheria za ujenzi na kuchangia uharibifu wa mazingira na sura ya jiji la Mombasa.

Katana aliongeza kuwa hali hiyo inahatarisha maisha ya jamii hasa wakati kunapozuka majanga kama vile moto kwani maafisa wa kuzima moto hushindwa kukabiliana na moto huo kutokana na ukosefu wa barabara ya kutosha kwenye eneo la tukio.

Aidha, alitahadharisha wananchi kufuata ramani ili wajue sehemu ya mabomba ya maji safi na chafu yanapopitia ili kuepuka kuvunjiwa majumba yao.

“Fuateni ramani wakati mnajenga ili kuepuka kuvunjiwa majumba yenu wakati wa ujenzi wa mabomba ya maji chafu,” alisema Katana.

Vile vile, alisisitiza kuwa hali hii huchangia mafuriko katika sehemu hizo wakati wa mvua.

Wakati huo huo, waziri wa ardhi Mombasa Francis Thoya alisema hawatayabomoa majumba hayo, ila sheria zitafuatwa kurudisha nidhamu ya jiji.

Wakuu hao waliyasema hayo wakati wa mkutano wa kujadili mpangilio wa jiji la Mombasa siku ya Jumatano.