Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amesema hatakubali kamwe sekta ya afya kurudishwa kwa serikali kuu tena.
Akiongea mnamo siku ya Jumamosi katika hospitali ya rufaa ya Kisii wakati kamati ya afya ya seneti, ikiongozwa na daktari Wilfred Machage, ilipotembelea hospitali hiyo ili kuona mabadiliko ambayo yamefanywa na serikali ya kaunti, Ongwae alisema tangu sekta hiyo iwe chini ya usimamizi wa serikali za kaunti, mabadiliko yameonekana pakubwa ikilinganishwa wakati sekta hiyo ilikuwa chini ya serikali kuu.
“Tangu sekta hiyo iwe nchini ya serikali za kaunti, hospitali hii imebadilika pakubwa maana mashine za CT scan nimeleta kwa hospitali hii ya rufaa ya kisii, mashine ya Digital Diagnosis na ile mashine ya Dialisis ziko, kwa hivyo hatutakubali sekta hiyo kurudishwa kwa serikali kuu tena,” alisema gavana Ongwae.
“Tunaomba sekta hiyo ibaki kuwa chini ya uongonzi wa serikali ya kaunti ili huduma iendelee kama ilivyokuwa imeanza,” aliongezea Ongwae.
Matamshi ya gavana yaliungwa mkono na seneta wa kaunti ya Kisii Chris Obure, ambaye pia alisema kama seneta hatakubali sekta hiyo kisimamiwa na serikali kuu.
Hii ni kufuatia na mswaada ambao ulipelekwa katika bunge la kitaifa kutaka sekta hiyo kurudishwa kuwa chini ya serikali kuu, huku akiwaomba wabunge kutokubali kamwe maana tangu ugatuzi kuanzishwa, mabadiliko yamekuwa kwa kiasi kikubwa na wananchi wameanza kufurahia matunda ya ugatuzi.
“Kulingana na utafiti nimefanya kwa wakaazi wa kaunti hii ya Kisii, mabadiliko yameonekana hasa kwa afya na wananchi wanaendelea kufurahia matunda hayo,” alihoji seneta Obure.