Jamii ya Gusii imetakiwa kutafuta ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa saikolojia wanapokumbwa na msongo wa mafikira.
Hii ni badala ya kukaa upweke hali ambayo hufunya baadhi ya watu kujiua.
Visa vya watu kujitoa uhai kwenye mitaa mingi mjini Kisii vimeripotiwa mara kwa mara na vingi vyao vimechangiwa na baadhi ya wakazi kunyamazia shida zao bila kushauriana na jamaa zao.
Kwa mujibu wa naibu chifu wa kata ndogo ya Nyaura katika eneo la Kiogoro, Yobes Mose, sharti watu wawe makini wanapoona mienendo ya mmoja wa jamaa zao imeanza kubadilika na kuanza kujitenga mara kwa mara.
Mose, akiongea siku ya Jumanne, alisema kuwa wengi wa wakazi wamejipata kwenye mshangao kwa kushtukia mmoja wao amejinyonga au amekunywa sumu.
Alishauri wakazi na jamii kwa jumla kuripoti visa vya utata pindi vinapogundulika miongoni mwao kwa mamlaka husika kama vile kwa ofisi za chifu ili kutafutiwa suluhu kwa wajuzi na wataalamu wa masuala ya saikolojia.
Mose alisema haya siku chache tu baada ya visa viwili sampuli hiyo kutokea kwenye eneo lake la utawala akitoa mfano wa karibu zaidi ambapo mzee mmoja alijitoa uhai kwa kujirusha kisimani baada ya kutengwa na familia yake kwa kile alichodai kuwa mzozo wa ardhi.