Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya polisi imetakiwa kutumia njia na mbinu ambazo zinaheshimu haki za binadamu wanapopambana na uhalifu kwenye mitaa mbalimbali katika mji wa Mombasa.

Akihutubia umati wa maafisa wa serikali kuu, na maafisa wa kaunti pamoja na hadhara katika uwanja wa umma wa Mombasa, siku ya Jumanne, kwenye hafla ya Mashujaa, mbunge wa eneo bunge la Mvita Abdulswamad Nassir, alisema kuwa idara ya polisi kwenye Kaunti ya Mombasa imekuwa ikitumia njia mbaya za kuwatafuta wahalifu ambayo huenda kinyume na haki za umma.

Nassir aliitaka idara hiyo kutumia mbinu zinazokubalika kisheria kupigana na uhalifu na kukoma kuwapiga wakazi kwa kizingizio cha kuwatafuta wakora.

Mbunge huyo alihimiza usimamizi wa idara hiyo kutoenda kinyume na katiba kwa vile jukumu lao ni kuwalinda wananchi.

“Mafisaa wa polisi wanafaa kufuata utaratibu wa kisheria kuwatafuta wahalifu ni si haki kuwajumuisha wakazi wote na kuwadhulumu bila sababu. Wazazi nao wanapaswa wawe katika mstari wa mbele kuwaelekeza watoto wao,” alisema Nassir.

Alishauri idara ya polisi kuweka uhusiano mwema na wakazi badala na kuwa na uhasama baina ya maafisa na wakazi, ili iwe rahisi kwa idara hiyo kukusanya taarifa za uhalifu na kuwapa umma moyo wa kutoa ripoti kwao bila uoga.

Haya yanajiri siku kadhaa baada ya wakazi kutoka mitaa mbalimbali ya jiji hilo kutoa lalama za kudhulumiwa na maafisa wa polisi wanapokuwa wakiwasaka magenge ya uhalifu.