Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa eneo la Pwani sasa wanadai kuwa serikali ina njama ya kuhakikisha kuwa ardhi ya pwani inatolewa kupitia Wizara ya ardhi iwapo sheria tata kuhusu ardhi ya jamaii itapita katika bunge la kitaifa.

Hii ni kutokana na ripoti kuwa asilimia 70 ya ardhi yote ya pwani iko chini ya usajili wa ardhi ya umma.

Kulingana na viongozi hao, iwapo swala hilo halitatatuliwa, basi wakazi wa eneo la Pwani watabaki kuwa maskwota kwani swala la kutatua mizozo ya ardhi linazidi kudidimizwa.

Akiwahutubia wakazi katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Jumapili, Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa alisema kwamba hatua hiyo ina dhihirisha wazi kuwa mtu yoyote anaweza kuomba na kupewa ardhi bila ya wenyeji kuhusishwa.

“Tunasikitishwa na hatua ya serikali jinsi inavyotaka kutatua maswala ya ardhi kwa kudai kuwa ardhi za Pwani ziko katika usajili wa ardhi za umma,” alisema Aisha.

Bi Jumwa amesema kwamba iwapo sheria hiyo haitafanyiwa marekebisho zaidi, basi swala la mizozo ya ardhi halitapa suluhu la kudumu.