Rais Uhuru Kenyatta amehimizwa kumtimua Prof Jacob Kaimenyi katika wadhfa wa Wizara ya Elimu kutokana na kushuhudiwa kwa visa vingi vya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa.
Kulingana na kiongozi wa vijana eneo la Kisauni Maxwell Masai, iwapo Rais Kenyatta atachukua hatua hiyo, basi sekta ya elimu itaimarika kwa kiwango kikubwa na swala la udanganyifu wa mitihani ya kitaifa litadhibitiwa.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa katika mkutano na wadau mbalimbali wa elimu, Masai alisema kwamba sekta ya elimu imesambaratika pakubwa kwani kukithiri kwa udanganyifu wa mitihani ya kitaifa kunadunisha elimu nchini.
Bw Masai amependekeza Kaimenyi kuondolewa katika wadhfa huo kwa kushindwa kuidhinisha sheria kali iliyokabiliana na udanganyifu wa mitihani, huku akisema kwamba hawatakubaliana na matokeo ya mitihani ya kitaifa itakayotangazwa mwaka ujao.
“Tunamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua za dharura na kumuondoa Waziri wa Elimu Prof Jacob Kaimenyi katika wadhfa wa uwaziri wa elimu kwa sababu jinsi wanafunzi na walimu wanavyoshirikiana katakana udanganyifu wa mitihani kumeonyesha wazi kwamba sekta hiyo imesambaratika,” alisema Masai.
Kauli ya kiongozi huyo imejiri baada ya walimu 12 kutoka shule ya msingi ya Star of the Sea mjini Mombasa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kushiriki katika udanganyifu wa mtihani wa KCPE.