Wananchi wa Songhor katika kaunti ndogo ya Muhoroni wameombwa kuzingatia usafi hasa nyakati hizi za mvua, ili kuepukana na maradhi yanayo sababishwa na mazingira machafu.
Katibu mkuu wa kundi la Wafanyakazi wa Afya ya Jamii, Community Health Workers (CHW) eneo hilo, Ann Chevali aliwasihi wakazi kudumisha usafi ili kujikinga na maradhi.
“Lazima kila familia ichimbe choo ilikusaidia kudumisha usafi,” akasema Chevali.
Wakazi hao pia wamehimizwa kufungua mitaro ya kupitishia maji chafu ambayo hufungana nyakati za mvua.
Chevali pia aliwaomba wakazi kufyaka nyasi iliyomea karibu na boma zao ili kufukusa mbu.
“Huu ni wakati wetu kama wakazi kuchimba mitaro ili maji taka yaweze kupita upesi,” akasema Chevali.
Chevali ambaye alikua akihutubu kwenye mkutano wa wanachama wa CHW mapema leo, amewataka wamama kuwa katika mstari wa mbele kwenye harakati za kuimarisha usafi na kutunza mazingira wanamoishi.
“Janga lolote linapotokea sisi kama wa mama huadhiriwa sana,” akahoji Chevali.