Share news tips with us here at Hivisasa

Wadau wa sekta ya uchukuzi mjini Mombasa wamelalamikia kukithiri kwa misongamano ya magari ya uchukuzi wa migizo katika eneo la Jomvu kaunti ya Mombasa.

Kwenye kikao cha kujadili jinsi ya kukabiliana na misongamano hiyo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Katibu wa Chama cha Wachukuzi wa masafa marefu cha ‘Trackers Union’ Ahmed Omar, kuendelea kushuhudiwa misongamo mikubwa katika eneo hilo huenda kukasambaratisha shughuli za uchukuzi.

Omar alisema kwamba iwapo hakutapatikana suluhu ya haraka, basi usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa kuelekea jijini Nairobi na nchi jirani utacheleweshwa kwa muda mrefu kutokana na misongomano ya magari mara kwa mara.

“Tumejadiliana mengi ila bado tuko na changamoto kubwa sana ya kudhibiti msingamano ya magari katika barabra zetu hizi za kuelekea Nairobi. Kwa sababu barabara yenyewe ni ndogo na magari yanayotumia barabara ni mengi. Tutaendelea kujadiliana katika vikao vyetu mpaka tupate suluhu la kudumu," alisema Omar.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na wahudumu wa Tuk tuk katika kaunti ya Mombasa Obedi Muruli, kukithiri kwa misongamano ya magari ya mizigo mara kwa mara kumechangiwa na kuzembea kwa baadhi ya viongozi wa halmashuari ya bandari ya Mombasa kutokana na kutoa mizigo kwa wakati usiofaa.

Aidha, aliitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuingilia kati swala hilo kwa kuishinikiza halmashauri ya barabara kuu nchini Kenha kuibuka na mbinu itakayoidhibiti misongamano hiyo katika eneo la Jomvu, mjini Mombasa.

“Misongamano ya magari ya uchukuzi ya mara kwa mara imesababishwa na kuzembea kwa viongozi wa halmashuri ya bandari ya Mombasa kuchelewesha kutolewa kwa mzigo ya kusafirishwa kwa wakati mwafaka, ikiwa watalitatua hilo, basi misongamano ya magari ya uchukuzi itapungua,” alisema Muruli.