Zaidi ya mabango 40 ya waganga 'bandia' yameng'olewa katika baadhi ya barabara za jiji la Mombasa kwenye oparesheni iliyoongozwa na machifu wa Tononoka na Mwembe Tayari.
Kulingana na chifu wa Tononoka Mwinyi AbdulAziz, oparesheni hiyo imeendeshwa baada ya agizo la kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa wiki mbili zilizopita, ambapo alitaka kung’olewa kwa mabango yote yaliyowekwa na waganga haswa kufuatia ripoti za utapeli.
Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Alhamisi, AbdulAziz alisema wameendesha oparesheni hiyo katika barabara za Tononoka-Bondeni, Sega, Haile Selassie miongoni mwa mitaa mingine ya lokesheni hizo, lengo kuu ikiwa kuangamiza kabisa biashara hiyo mjini Mombasa.
Aidha, alitoa onyo kali kwa wanaojihusisha na biashara hiyo akisema serikali iko macho na watakaopatikana hawatosazwa.
Haya yanajiri huku chama cha madaktari wa miti shamba eneo la Pwani NATHEPA wakiunga mkono kuendelezwa kwa oparesheni hiyo ili kuwaondoa matabibu tapeli wanaohadaa wakenya.