Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tume ya kukabiliana na ufisadi nchini tawi la Nakuru sasa inatarajiwa kuanza uchunguzi wake mara moja kuhusiana na madai ya ufisadi na utumizi mbaya ya fedha za umma ambao umedaiwa kutekelezwa na maafisa wa serikali ya kaunti ya Nakuru.

Ahadi hiyo imetolewa na afisa wa tume hiyo tawi la Nakuru Gilbert Lukoba baada ya kundi la wakazi wa Nakuru kufanya maandamano ya amani mjini Nakuru hadi kwenye afisi za tume hiyo.

Ni maandamano yaliyojiri baada ya ripoti ya mkaguzi wa hesabu kuonyesha kuwa kiwango kikubwa cha fedha kimefujwa na maafisa wa serikali wa kaunti ya Nakuru kwenye mwaka wa kifedha wa 2013 hadi 2014.

"Tumepokea malalamishi yenu na tutayasoma, tuyatathmini na tuyachunguze na tutawajibu kulingana na sheria ambayo imebuni tume hii," alisema Lukoba.

Abdul Noor, ambaye aliongoza maandamanao hayo aliweka wazi kwamba alitaka majina ya watu wanaodaiwa kuhusiaka katika ufisadi kuwekwa wazi na watu hao kuchunguzwa na pia kuchukuliwa hatua kali za kisheria endapo watapatikana na kosa hilo.

"Baada ya kukabidhi majina haya kwa tume ya kukabiliana na ufisadi, tunataka maafisa wa tume hii wachukue hatua ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani. Mtu mmoja hawezi kutumia shilingi elfu arobaini kulala hotelini kwa siku moja, hizo  ni fedha ambazo zingetumiwa kuwajiri vijana watatu au wane zinatumika kwa njia za anasa," alilalama Noor.

Noor pia alimtaka afisa mkuu anayesimamia kitengo cha fedha kwenye kaunti ya Nakuru kujitokeza na kuelezea wakazi wa Nakuru kuhusiana na jinsi fedha za umma zilivyotumika

"Tunataka afisa mkuu anayehusika na maswala ya fedha aeleze kaunti ya Nakuru na wananchi kwa jumla jinsi fedha za wanachi zinavyotumika kwa sababu wananchi ndio wanaotozwa ushuru kupitia kwa kodi mbalimbali. Ni vizuri kwa wanachi kujua iwapo fedha zao zinatumiwa vizuri," alikariri Noor.