Ofisi ya wizara ya ardhi katika serikali ya kaunti ya Kisii imefungwa kwa majuma mawili yajayo ili stakabadhi za ardhi zipangwe kidijitali kama njia mojawapo ya kuzuia unyakuzi wa mashamba katika kaunti hiyo.
Akizungumza na wanahabari mnamo siku ya Ijumaa jioni katika ofisi ya gavana James Ongwae mjini Kisii, Waziri wa mawasiliano nchini ambaye pia anashikilia wizara ya ardhi kwa mda Fred Matiang’i aliamua kufunga ofisi hiyo ili stakabadhi za mashamba kupangwa kidijitali na kuzuia unyakuzi wa mashamba katika kaunti hiyo.
“Ili kuzuia unyakuzi wa mashamba katika kaunti ya Kisii ambao umeshuhudiwa kwa mda mrefu, sharti stakabadhi zipangwe kidigitali,” alisema Matiang’i.
“Stakabadhi hizi za mashamba hazijawai kupangwa tangu nchi ya Kenya ijinyakulie Uhuru kwa miaka 53 iliyopita, ndio nikaamua ofisi hiyo ifungwe kwa wiki mbili ili kila kitu kikipangwa kidigitali, basi ofisi itafunguliwa tena hatutaki visa vya unyakuzi wa mashamba kushuhudiwa tena katika kaunti ya Kisii,” aliongezea Matiang’i.
Wakati huo huo, gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alisema kuwa stakabadhi hizi zikipangwa kidijitali hakutakuwa na changamoto za mashamba kwa kaunti yake huku akisema kuwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii wale wanasomea taaluma ya technolojia watakuja kwa ofisi hiyo ya ardhi iliyofungwa na kuorodhesha na kupanga stakabadhi hizo kidijitali .
Wanafunzi wa chuo chuo chetu cha Kisii wale wanasomea masuala ya tekinolojia watakuja kuzipanga stakabadhi hizo,”alisema gavana Ongwae.