Wenye mbwa katika Wilaya ya Ogembo, Kaunti ya Kisii wamehimizwa kutibu wanyama hao na kuhakikisha kuwa wamefanyiwa chanjo kila mwaka ili kuzuia kichaa cha mbwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa kitengo cha kushughulikia afya ya wanyama katika Wilaya hiyo Dkt. Jared Manyeki akiongea siku ya Jumanne, aliwasihi wafugaji haswa wa mbwa kutilia maanani afya ya mbwa wao ili kuepuka uambukizaji wa maradhi ya kichaa cha mbwa.

Dkt. Manyeki alitaja maradhi hayo kuwa hatari zaidi endapo mbwa atamng'ata binadamu na hata husababisha kifo iwapo mwathiriwa hatapata matibabu ya mapema.

"Iwapo mtu ameumwa na mbwa sharti atafute msaada wa daktari haraka iwezekanavyo ili kuzuia sumu ya mbwa kusambaa mwilini na aghalau kusababisha mwathiriwa kubweka kama mbwa,” alishauri Dkt. Manyeki.

Amesema haya siku tatu tu baada ya muungano wa madaktari wa wanyama nchini kusherehekea siku kuu ya Madaktari hao ulimwenguni (World Vetenery Day) huko Kaunti ya Busia mwezi Aprili 25 Jumamosi ambapo aliwataka wafugaji kujitokeza kila mwaka kusherehekea siku hiyo kwa kutibu wanyama wao kwa jumla.

Mbali na himizo hilo, Dkt. Manyeki alistajaabikia kiwango kidogo cha wenye mbwa vijijini ambao hutibu mbwa wao huku akiwataka kuiga wenzao wa mijini ambao alitaja kuwa wameonyesha kuwajibikia mifugo yao, kwani siku za hivi karibuni wakaazi wa maeneo hayo ya Ogembo na viunga vyake wamelalamikia kurandaranda kwa mbwa ambao huenda wakawauma watu nyakati za usiku na kuwadhuru kiafya.