Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wadi ya Kiptagich katika eneo bunge la Kuresoi Kusini James Tuei, amewahakikishia wakazi wa Kuresoi kuwa Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua hajawatenga kimaendeleo.

Tuei amesema kuna porojo zinazoenezwa na watu fulani dhidi ya Gavana Mbugua lakini akasisitiza kuwa serikali yake haijalibagua eneo bunge ya Kuresoi kusini na kaskazini.

Akiongea afisini mwake Jumanne asubuhi, Tuei alikanusha madai kuwa gavana Mbugua ameyatenga maeneo hayo mawili.

Mwakilishi huyo alisema kuwa gavana Mbugua amezindua miradi mingi ya maendeleo katika maeneo hayo mawili na kuwataka wanaoeneza porojo hizo kukoma kuwapotosha watu.

“Kuna baadhi ya watu wanashinda wakizunguka Kuresoi wakiambia watu kuwa serikali ya Nakuru imewatenga kimaendeleo lakini hiyo ni porojo tupu. Mimi kama mwakilishi wadi nimeandamana na gavana Mbugua marakadhaa akienda Kuresoi kuanzisha miradi ya maendeleo,” alisema.

“Mimi ninafanya kazi kwa karibu sana na Gavana Mbugua na ninavyojua si mtu wa kubagua watu kwa misingi ya kikabila kwa sababu Nakuru ni ya makabila yote,” akasema.