Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mzee wa miaka 63 aliyefikishwa kwa mahakama moja mjini Nakuru siku ya Jumatatu kwa kosa la kumiliki pombe haramu alijitetea kwa kusema aliandaa pombe hiyo ili iweze kutumika kwenye sherehe.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa mshtakiwa huyo, John Kangor, alinaswa na lita tano za busaa siku ya Jumamosi katika eneo la Banita, Kaunti ya Nakuru, na isitoshe, hakuwa na kibali cha kuuza pombe hiyo.

Akijitetea mahakamani, mzee huyo alisema alikuwa amemuoza bintiye na aliandaa pombe hiyo aliyoitaja kama ya kienyeji ndiposa apokee mahari, hatua iliyo sambamba na utamaduni unaofuatwa na watu wa jamii yake.

Hata hivyo, alipelekea waliokuwa mahakamani kuangua kicheko baada ya kusema pombe hiyo iliyonaswa na askari bado haikuwa tayari.

Aidha, alidai kuwa huenda pombe hiyo ikawa tayari hii leo.

Hakimu mkuu, Joel Ng’eno aliyekuwa akisikiza kesi hiyo, alimwachilia huru kwa shtaka la pili huku akimtoza faini ya shilingi elfu tano kwa shtaka la kwanza.