Wakazi wa Manga wamemuunga mkono kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga kwa juhudi zake zilizo sababisha kutiwa mbaroni wezi sugu wa mifugo kutoka eneo hilo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari siku ya Alhamisi diwani wa zamani wa Manga Charles Omwana aliyewaongoza wakazi wa eneo hilo kumuunga mkono kamishnana huyo alisema kuwa juhudi za Onunga zimewasaidia sana wakazi wa Manga baada ya wezi sugu wa mifugo ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi kutiwa mbaroni. 

"Kamishna Onunga ameonyesha kujitolea kwake kupigana na wizi wa mifugo kwa kuwa tuliandamana naye siku ya Jumatano kwenye msako mkali uliofanikisha kupatikana kwa ng'ombe watatu kati ya kumi waliokuwa wamepotea na hata kupelekea kutiwa mbaroni kwa washukiwa watano watakaofikishwa mahakamani kutoa ushahidi wao," alisema Omwana.

Wakazi hao aidha walichukua fursa hiyo kumwomba kamishna Onunga kuwapeleka polisi zaidi katika eneo hilo ili wasaidie kuthibiti visa vya wizi katika eneo hilo. 

"Kwa kuwa wezi wa mifugo hutekeleza wizi wao kwa kuwa na ushirika mkubwa na watu wengi tungependa kumwomba kamishna Onunga kuwaleta polisi zaidi kwenye eneo la mpakani ili wasaidie kuthibiti visa vya mara kwa mara vinavyotokea hapa," alisema Omwana.