Mwanamme mmoja amepoteza maisha yake baada ya kugongwa na pikipiki akivuka barabara katika barabara ya Mwingi, Thika.
Mwanamme huyo mwenye umri wa makamu alikumbana na ajali hiyo alipokuwa akivuka barabara kuelekea kwenye shughuli zake za kila siku.
Kulingana na walioshuhudia, mwendeshaji pikipiki huyo alijaribu kadri ya uwezo wake kumhepa, bila juhudi zake kuzaa matunda huku akimrusha na kuanguka ndani ya shimo la mawe na kujigonga kichwa vibaya na kuumia.
“Huyo mtu alipokuwa akivuka aliona hakuna magari bila kujua kuwa kuna pikipiki iliyokuwa ikija kwa mwendo wa kasi, pale ilimgonga na kumtupa mbali,” alisema Mary Mwangi, mmoja wa wachuuzi aliyeshuhudia ajali hiyo.
Mwanamume huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Thika Medical, na kisha kupelekwa hospitali kuu ya Kenyatta baada ya afya yake kudorora, lakini aliyapoyeza maisha yake saa chache baada ya kufikishwa humo.
Pikipiki iliyomgonga mwanamme huyo inazuiliwa katika kituo cha polisi cha Thika, huku mwenye pikipiki hiyo akiendelea kusakwa na polisi baada ya kutoweka.