Mwenyekiti wa bodi ya elimu kaunti ya Kisii Henry Onderi amesema shule za Kisii hufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa kutokana na wazazi kutolipa karo kwa watoto wao kwa wakati ufaaao.
Akizungumza na wanahabari mnamo siku ya Ijumaa katika mji wa Kisii, mwenyekiti huyo aliwakosoa wazazi kwa kutolipia watoto wao karo ya shule mapema na wanafunzi kufukuzwa nyumbani, jambo ambalo alisema huchangia wanafunzi kutofanya vyema katika mtihani.
“Wanafunzi wanapofukuzwa kuleta pesa kutoka makwao wengine hupoteza wakati njiani kuchukua pesa huku wakarandaranda na kupoteza wakati wa masomo, naomba wazazi kulipa pesa kwa watoto wao wakati unaofaa ili shule za Kisii zifanye vyema katika mtihani,” alihoji Onderi.
Matamshi yake yaliungwa mkono na mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya Pangani Pancificah Omboki, ambaye pia alikuwa na mwenyekiti huyo na kusema kuwa sharti wazazi wawalipie watoto wao karo kwa wakati ufaaao.
Aidha, mwenyekiti huyo aliwakosoa baadhi ya wazazi kuwachukuwa watoto wao shule za nje kando na zile za Kisii, ambazo hufanya vyema na kusema kuwa hiyo ni njia moja ya kuchangia shule za Kisii kuendelea kufanya vibaya.
“Mkitaka shule zetu za Kisii kufanya vyema katika mitihani, sharti watoto wenu wasome hapa Kisii na kuweka kando mbinu ya kuwachukuwa shule za kaunti zingine,” aliongezea Onderi.
Naye gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alisema kuwa serikali ya kaunti yake inajaribu iwezalo kuhakikisha viwango vya elimu vimepanda katika eneo hilo, huku akisema mwaka huu watajenga madarasa 90 ya ECD kwa wadi 45.