Chifu wa eneo la Tala bwana Pius Nzioka amewaonya wamiliki wa vyumba vya video dhidi ya kukubalia watoto kuingia humo na kutazama filamu zisizofaa watoto wa umri wao.
Hii ni baada ya walimu wa eneo hilo kulalamikia hatua ya idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi kukwepa darasa na kwenda kuona video.
Nzioka amesema visa hivyo vimeripotiwa zaidi katika soko za Tala, Nguluni na Komarock, huku akiwataka wamiliki wa vituo hivyo kuzingatia sheria zilizowekwa.
Nzioka alitishia kufanya msako pamoja na askari wa utawala katika sehemu hiyo ili kuhakikisha kuwa wanaokiuka sheria wanatiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka.
Vileviile chifu huyo alitoa mwito kwa wazazi katika eneo hilo kutowaachia walimu jukumu la kutunza watoto na kuwataka kuwajibika kikamilifu.
"Ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha kuwa anawajibika katika malezi ya watoto wake, wazazi wengi wamepuuzia wajibu wao na kuwaachia walimu jukumu la kuwatunza watoto," alisema Nzioka.
Walimu wakuu wa shule za msingi katika sehemu hiyo wamedai kuwa idadi kubwa ya wanafunzi huwa hawafiki shuleni, na kuwa baada ya kufanya uchunguzi wamebaini wanafunzi hao huondoka nyumbani wakidai kwenda shuleni lakini huingia na kushinda kwenye vyumba vya video vilivyozagaa eneo hilo.