Mahakama kuu mjini Mombasa imempa mwanamume wa umri wa makamu hukumu ya kifo kwa kosa la kumuua mpenzi wake kutokana na ugomvi wa kinyumbani.
Inadaiwa kuwa mshukiwa huyo, Abdullahi Wada, alitekeleza kitendo hicho cha kumuua mchumba wake, Milga Abdullahi, aliyekuwa akihudumu kama afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Makupa mwaka wa 2013.
Kulingana na ushahidi wa kesi hiyo, mshukiwa huyo aliamua kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi akisingiziwa kushambuliwa kwa kukatwa katwa mikono kwa kisu, madai mahakama iliyapinga na kupatikana na hatia ya mauaji.
Wakili wa mshukiwa Gerald Magolo alielezea mahakama kuwa mshukiwa ni mwanamume wa umri wa miaka 36 na ana mke na watoto wawili na mahakama inafaa kumsamehe kwani mteja wake hajawahi kosa vikao vya mahakama na anafaa kupewa kifungo cha nje.
“Ningeiomba mahakama imuachilie mteja wangu na kumpa kifungo cha nje kwa sababu mteja wangu yuko na mke na watoto wawili wanaohitaji usaidizi wake kama mzazi katika familia. Iwapo atawekwa gerezani, basi familia yake itapitia hali ngumu ya maisha kwa sababu mke wa mteja wangu bado hana ajiri,”Magolo aliieleza mahakama siku ya Jumatatu.
Jaji wa mahakama hiyo Matin Muya alidai kuwa kesi hiyo ina uzito kulingana na jinsi ushahidi uvyokuwa ukitolewa katika mahakama hiyo, na mshukiwa anafaa kutumikia hukumu hiyo.
“Ushahidi uliotolewa umebaini kuwa mshukiwa alitekeleza kitendo hicho cha mauaji ya mchumba wake kwa mzozo wa kifamilia na sheria hairuhusu mwananchi kuchukua hatua ya kutoa uhai wa mwenzake,” alisema Jaji Muya.
Hata hivyo, ametoa muda wa siku nne za wakili wa mshukiwa kukata rufaa ama mshukiwa kutumikia hukumu hiyo ya kifo.