Share news tips with us here at Hivisasa

Madereva wa magari ya aina ya 'probox' mjini Kisii wameomba serikiali ya kaunti kuwatengea mahala kama kituo chao cha magari ili kukuza sekta yao ya uchukuzi.

Wito huo umetolewa baada ya kusemekana kuwa wahudumu hao hawafanyi uchukuzi wao inavyostahili kwani wengi hawajui mahala gari hizo zinaegeshwa.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, mwenyekiti wa magari hayo aina ya 'probox' mjini Kisii Elijah Bosire na wahudumu wengine walisema wao hutozwa ushuru kiwango sawia na wahudumu wengine wa matatu na kuomba kutafutiwa mahala watakakoweka kituo chao cha magari ili kukuza sekta yao ya uchukuzi.

Kulingana na mwenyekiti huo, kuanzia juma lijalo, vituo vyote vya magari katika kaunti ya Kisii vitasajiliwa katika shirika lililoundwa siku ya Jumatano kwa jina Kisii Matatu Welfare Association ili kubaini magari yote yafanyalo uchukuzi katika kaunti nzima ya Kisii jambo ambalo wameshangazwa nalo kwani hawana kituo cha kusajiri.

“Tunaomba serikali ya kaunti ya Kisii kututengenezea kituo chetu kwani tumeshindwa la kufanya na tunatozwa ushuru ingawa tunaegesha magari kando mwa barabara. Tunaomba tutengewe mahala ili iwe rahisi kwetu kujisajili kwa shirika la uchukuzi katika kaunti ya Kisii,” alisema Peterson Ochako, dereva.

Wahudumu hao huwa wanaegesha magari yao kilomita moja unusu kutoka kwa vituo vingine vya magari vilioko mjini Kisii jambo ambalo wameomba kusuluhishwa kwa haraka.

“Mimi napendekeza ikiwa hatutatengewa kituo chetu, tunastahili kutozwa kiwango kidogo cha ushuru ikilinganishwa na kile wahudumu wengine hutozwa kwani sio watu wengi wanaojua kuwa tunabebea mahala hapa,” alisema Bosire.