Waendeshaji bodaboda katika kituo cha matatu cha Maili Sita, wamesema wanahofu ya uwezekano wa kuzuka kwa mkurupuko wa maradhi miongoni mwao kwasababu ya ukosefu wa vyoo katika kituo hicho.
Wakizungumza siku ya Jumanne, wahudumu hao walisema kwamba wamekuwa wakijisaidia katika vyoo vya hoteli zilizo karibu, lakini sasa wamefungiwa milango na kulazimika kutafuta kichaka cha karibu kujisaidia.
Mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda katika eneo hilo Joseph Macharia, alisema kuwa sio wao tu ambao huwa wanateseka kwa kukosa choo, kwani pia wateja wao hulazimika kujisaidia vichakani.
“Sio mara moja nimebeba mteja hapa, hata mwanamke, kisha tukifika njiani ananiambia nimshukishe kwanza ajisaidie,” alisema Bw Macharia.
Hata hivyo, walidokeza kwamba kulikuwa na maelewano na afisi ya fedha za ustawi wa maeneo bunge ya eneo bunge la Bahati kwamba watajengewa choo mwaka uliopita, ahadi ambayo walisema haijatimia
“Tuliambiwa kwamba ujenzi wa barabara hii ya Nakuru-Maili Kumi ukikamilika tutajengewa choo karibu na mpaka wa shule hii ya Kiamaina. Bado tunasubiri,” alisema Macharia
Wahudumu hao walisema hawaoni ugatuzi umewaletea faida gani, kama kupata choo imekuwa ni tatizo kubwa.
Mwakilishi wa wadi ya Kiamaina, Samwel Kamau, alisema bado anashugulikia swala hilo, na punde litakapomalizika vyoo vitajengwa katika eneo hilo.