Huku uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 ukikaribia, viongozi wa siasa kutoka maeneo tofauti katika eneo zima la Pwani hawajaachwa nyuma katika harakati za kuwa na maandalizi ifikiapo wakati huo, huku wakijiweka pamoja kwa azimio la kuwa na chama kimoja cha siasa kutoka eneo hilo.
Wabunge hao zaidi za kumi na watatu, ambao walikusanyika jijini Mombasa Jumatu, walisema kuwa hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa eneo la Pwani lina usemi katika masuala si, tu ya siasa bali Nyanja zote hasa masuala ya kupata kazi za serikali pamoja na uboreshaji wa masuala ya uchumi kwa jumla.
Wakiongozwa na mbunge wa eneo bunge la Kaloleni, Mwinga Gunga, wabunge hao walisistiza kuwa ili eneo la Pwani kuwa na sauti moja sharti waunde chama cha siasa ambacho kitakuwa kikitetea maslahi yanawakumba wakazi wa Pwani ambao wanadai kwa mara nyingi wamekuwa wakitumiwa na maeneo mengine kwa manufaa ya binafsi na kusahaulika baada ya kila uchaguzi tangu nchi ya Kenya kujipatia uhuru.
Hata hivyo, bado hawajataja jina la chama hicho na kusema kuwa bado wanaendelea kuweka mikakati ya kuona kila kiongozi kutoka eneo la Pwani anasimama na wao na kuona jinsi ya kuendeleza ajenda yao baada ya kukubaliana na viongozi wote kwa jumla ambao wanatoka kaunti zote za Pwani.