Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Bodi inayosimamia filamu nchini imetoa onyo kali kwa wanaosambaza filamu za ngono na zile hazijasajiliwa sambamba na zisizoambatana na katiba kuwa watakabiliwa kisheria.

Kulingana na afisa mkuu wa bodi hiyo Ezekiel Ole Mutua, taifa hili limekumbwa na changamoto za maadili potovu kufuatia kukithiri kwa filamu haramu zinazochangiwa na wafanyibiashara ghushi pamoja na wageni wanaoingia humu nchini.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu baada ya mkutano na Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, Mutua amesema kwamba kuenea kwa filamu hizo nchini na hususan katika ukanda wa Pwani kumesababisha hata vijana wadogo kujiunga na maswala ya itikadi kali kufuatia mafunzo wanayopokea kutoka kwa filamu hizo.

Mutua amewataka wanachi kutoa habari kwa maafisa wa bodi hiyo sambamba na maafisa wa polisi kuwatia nguvuni wanaoendeleza biashara hiyo potovu ama kuwashawishi vijana wadogo kushiriki filamu za ngono ili taifa hili kuwa na maadili mema.

"Tunawaonya wale wanaoingiza filamu za ngono na kufanya filamu na wanyama kuwa maafisa wetu kwa ushirikiano na maafisa wa polisi watakabiliwa na kubadilisha sura ya nchi kuwa yenye watu wa maadili mema," alisema Mutua.

Maafisa wa bodi hiyo wameahidi kuzuru mashinani na kuyakagua maduka, vituo vya sanaa za filamu na vibando vidogo vinavouza filamu kwa ushirikiano na maafisa wa polisi ili kuona kwamba jamii haipotoki kimaadili.