Wakulima wanaofuga samaki katika kaunti ya Nyamira wana kila sababu yakutabasamu baada ya serikali ya kaunti hiyo kutenga Sh2m, kununua samaki watakao fugwa kwenye kidimbwi cha Kitaru katika eneo la Mekenene.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumanne kule Nyamaiya, Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama alisema kuwa wakulima ambao wamekuwa wakifuga samaki watafaidi pakubwa kwa kununua samaki hao kwa bei nafuu ili kuendeleza biashara zao.

"Wakulima ambao ni wafugaji wa samaki watafaidi pakubwa kutokana na mpango huo kwa kuwa wataweza kununua samaki hao kwa bei nafuu," alisema Nyagarama.

Gavana Nyagarama alisema kuwa mradi huo utangoa nanga mwezi Novemba baada ya kufanya udadisi katika eneo hilo.

"Mradi huo utangoa nanga mwezi wa Novemba mwaka huu baada ya udadisi kufanyika katika maeneo hayo. Mradi ambao tunanuia kuuanzisha utaweka kaunti yetu miongoni mwa kaunti zenye uzalishaji na uuzaji wa juu wa samaki,” alisema Nyagarama.

Gavana huyo alisema kuwa serikali yake itakuwa ikinunua samaki hao kutoka kwa wakulima na kisha kuwauza nje.

"Serikali yangu itanunua samaki hao moja kwa moja kutoka kwa wakulima na kisha kuwauza kwenye mataifa ya kigeni,” alisema Nyagarama.

Haya yanajiri baada ya kaunti hiyo kuteuliwa kuandaa sherehe za maadhimisho ya siku ya chakula duniani hivi maajuzi.