Zaidi ya familia hamsini zilisalia bila makao baada ya moto kuzuka jumapili na kuteketeza nyumba katika eneo la Laini Saba, Kibera.
Imeripotiwa kwamba moto huo ulianza mwendo wa saa nne asubuhi na kusambaa kwa kasi, kabla ya kudhibitiwa masaa kadhaa baadaye.
Japo chanzo cha moto huo hakijabainika, wenyeji wanadai kwamba ulisababishwa na hitilafu za nguvu za umeme kufuatia utepetevu wa mkaazi mmoja aliyekuwa akitumia kifaa cha kuchemsha maji ambacho kililipuka.
“Moto ulianza saa nne asubuhi; nilikuwa katika duka langu niliposikia mlipuko nje na baada ya dakika chache, stima ikapotea. Nilichoshuhudia muda mfupi ni moshi mkubwa ishara kwamba moto ulikuwa umeanza,” alisema Daniel Mbithi, mmiliki wa duka ambalo liliteketea.
“Singeweza kuokoa chochote kwani moto ulisambaa kwa kasi sana. Ilinibidi nitoroke ili kuepuka madhara,”aliongeza Mbithi.
Mbithi alisema kwamba maafisa wa kuzima moto waliwasili takriban dakika thelathini baada ya moto kuanza, na hivyo kusaidiana na wakaazi kuudhibiti.
Kwa upande wake, Mohammed Bangwa ambaye ni mmiliki wa nyumba moja iliyoteketea alisema kwamba mshirika mbalimbali pamoja na wawakilishi kutoka afisi za viongozi walifika katika eneo la mkasa jumatatu na kuahidi kuwapa msaada waathiriwa.
“Kufikia sasa bado hatujapata msaada wowote, hata hivyo maafisa kutoka afisi ya mbunge wetu Ken Okoth, chifu wa eneo hili pamoja na maafisa wa shirika la msalaba mwekundu wamefika hapa na kuahidi kutusaidia,” alisema Bangwa.
Judith Nyaboke ambaye ni katibu wake mwakilishi wa wadi ya Laini Saba David Kitavi, alifika na kushudia hasara iliyotokea na kuhakiki kwamba waathiriwa watasaidia iwezekanavyo ili warejelee hali ya kawaida ya maisha.
“Tunasikitika pamoja na walioathirika na mkasa huu wa moto ambao umeacha takriban familia hamsini bila makao. Tumeanza mikakati ya kuwasaidia waathiriwa kwani tayari tumesajili majina yao ambayo tutawasilisha kwa msimamzi wa shughuli za wadi ambaye atayawasilisha tena mbele ya serikali ya kaunti ya Nairobi kupitia kwa bwana Kitavi,” Nyaboke alihakikisha.