Share news tips with us here at Hivisasa

Mchakato wa Jumuiya ya kaunti za Pwani sasa umepigwa jeki baada ya kampuni ya ushauri wa kiuchumi ya ‘Delloite and Touché’ kujitosa ndani ili kuunda mwongozo wa jinsi uchumi wa kaunti zote za eneo la Pwani utaimarishwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mwenyekiti wa muungano huo ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kwale Salim Mvurya alisema kwamba kampuni hiyo ya Delloite ina tajriba ya miaka mingi ya ushauri wa kiuchumi na ubunifu utakaoiwezesha Jumuiya hiyo kupiga hatua.

Mvurya alisema kwamba kongamano la kujadili mikakati mwafaka ya kiuchumi limepangwa kufanyika katika kaunti ya Kwale na litawajumuisha viongozi wa Kaunti zote za Pwani sawia na wasomi kutoka kaunti hizo kwa lengo la kujadiliana kuhusu jinsi kielelezo hicho kitakavyobuniwa ili kiafikie malengo ya muungano huo wa Jumuiya ya kaunti za Pwani.

“Kama viongozi wa muungano wa jumuiya ya kaunti za pwani, kupanga kongamano la kuwajumuisha wasomi na viongozi wa kampuni hiyo ili kuona kwamba tunapanga mikakati mwafaka ya kuimarisha uchumi wa eneo letu pamoja na kuafikia malengo yote ya ruwaza ya mwaka 2030,” alisema Mvurya.

Aidha, aliwataka wakaazi wa mjini Mombasa na eneo zima la Pwani kushirikiana na viongozi wao kwenye muungano huo ili katika siku za usoni waweke msingi thabiti wa kiuchumi katika kaunti zao na kuukabili viliyo umaskini katika Jamii.

Kongamano hilo la siku tatu litakalong’oa nanga hivi karibuni na kuwajumuisha wasimamizi wakuu wa mchakato wa ruwaza ya mwaka wa 2030.