Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Zaidi ya wakaazi elfu moja kutoka mtaa wa 'Dunga Unuse' eneo la Changamwe, Mombasa wamelalamikia kukumbwa na maradhi baada ya kufurushwa katika makaazi yao.

Kulingana na wakaazi hao, tangu kufurushwa kwao na bwenyenye mmoja aliyedai kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo ya hekari 500, wamekuwa wakiishi katika mahema ambayo walipewa na wahisani huku akisema kwamba changamoto wanazozipia na nyakati hizi za mvua huenda wakakumbwa na maradhi mengi.

Wakaazi hao wakiongozwa na Martin Gunjwa walisema serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa imewatenga licha ya wao kuwasilisha lalama zao kupitia kwa viongozi wao ili kuona wanapata msaada.

Bw Gunjwa alikashifu hatua hiyo na kusema kwamba baadhi ya maafisa tawala na viongozi wa kisiasa wanashirikiana na mabwenyenye kuwafurusha wakaazi katika ardhi zao kwa malengo yao binafsi.

Aidha, Gunjwa aliitaka serikali kuwatambua wakaazi hao na kuidhinishwa usaidizi wa haraka kwani wanaohofia maisha yao kwamba huenda wakaambukizwa maradhi kutokana na hali ngumu ya maisha wanaoyopitia.

“Tunaiomba serikali kuu na hii ya kaunti yetu ya Mombasa kututambua sisi wakaazi wa 'Dunga Unuse' baada ya kufurushwa kwa makaazi yetu," alisema.

"Tumetengewa nini ama lengo la serikali pia kutuona tukiangaika kwa sababu hatuna uwezo wa kupigana na bwenyenye huyu ila tunaomba serikali itutambue na kututengea mahali pa kuishi."

Mapendekezo ya wakaazi hao yamejiri baada ya bwenyenye mmoja kudai kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo na kuwafurusha pamoja na kuwavunjia nyumba zao yapata muda wa miezi miwili iliyopita.