Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir ametishia kuongoza maandamano mjini Mombasa kulalamikia dhuluma wanazotendewa na maafisa wa polisi katika kaunti hiyo.
Akizungumza katika eneo bunge la Mvita mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Abdulswamad alisema kwamba wakazi wa eneo bunge hilo wamekuwa wakihangaishwa na maafisa wa polisi kwa wakitiwa nguvuni na kuzuiliwa bila ya makosa yoyote.
Mbunge huyo alisema kwamba iwapo hali hiyo haitakomeshwa, basi wakazi hao watasambaratisha shughuli zote katika kaunti hiyo kwa kufanya maandamano makubwa ya kulalamikia dhuluma hizo.
“Tuko tayari kuandaa maandamano kutokana na dhuluma tunazozipitia zinachangiwa na maafisa wetu wa polisi, iwapo idara ya polisi haitaingilia kati swala hili na kubadili hatua zao za kufanya operesheni ya kiusalama,” alisema Abdulswamad.
Alisema kwamba ushirikiano kati ya maafisa wa polisi na wakaazi katika eneo bunge la Mvita na kaunti ya Mombasa kwa jumla umefifia kutokana na dhuluma hizo, huku akisema kwamba swala hilo linafaa kusitishwa.
Kwa muda sasa tangu misako ya polisi izinduliwe katika juhudi za kudhibiti uhalifu na ugaidi, wakazi wa kaunti hiyo wamelalamikia pakubwa dhuluma wanazotendewa na maafisa wa polisi.