Waziri wa ardhi katika kaunti ta Kisii Moses Onderi amewataka wakaazi wa Nyangweta kuwa na subira kwani kiwanda cha kusaga miwa walichohaidiwa kitaanzishwa hivi karibuni
Akiongea katika afisi yake, Onderi aliwahimiza wakaazi kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa kupinga maendeleo katika maeneo yao, kwani kufanya hivyo hudidimiza maendeleo katika maeneo husika.
Pia aliwataka kuchangamkia uwekezaji katika maeneo yao, na kukoma kutumiwa vibaya na wanasiasa ambao hawana maono ya kuwaendelezea uchumi katika maeneo wanamoishi.
Waziri huyo alikuwa anagusia swali aliloulizwa kuhusiana na madai kuwa baadhi ya. wanasiasa na wakaazi wa Nyangweta wamekuwa wakichochewa kupinga mradi wa kuanzishwa kwa kiwanda cha kuchakata miwa katika eneo hilo lililoko katika eneo bunge la Mogirango Kusini.
Aliongezea kuwa kamati kutoka kaunti ya Kisii ilishazuru eneo hilo ili kutathmini mradi huo wa ujenzi wa kiwanda cha miwa, ambacho huenda kikawa cha kwanza katika kaunti hiyo.
“Kiwanda hicho kikijengwa kitawafaidi vijana na wakaazi wa eneo hilo kwa kupata kazi mbalimbali ambazo zitawainua kiuchumi," alisema Onderi, huku akiwaonya wanyakuzi wa ardhi katika kaunti kuwa siku zao zinahesabiwa.
Kaunti ya Kisii ni ya tatu katika kilimo cha miwa baada ya mkoa wa Magharibi na ule wa Nyanza Kaskazini, na kujengwa kwa kiwanda hicho kutaimarisha upandaji wa miwa na kuboresha uchumi wa eneo la Gusii kwa jumla.