Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ya kuajiri walimu nchini TSC imesimamisha zoezi la usajili wa kuajiri walimu wa shule za umma za msingi na upili kote nchini.

Kulingana na Mkurugenzi wa Tume hiyo katika kaunti ya Mombasa, Ibrahim Rugut, tume hiyo imechukua hatua ya kusitisha zoezi hilo kwa muda baada ya mahakama kuu jijini Nairobi kutoa agizo la kusitishwa kwa zoezi hilo ili tume hiyo ishughulikie swala la kuwalipa walimu nyongeza yao.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rugut alisema kwamba kaunti ya Mombasa ilikuwa imetengewa nafasi 583 za walimu wa shule za umma, idadi ambayo walimu 531 walifaa kuajiriwa katika shule za msingi huku 52 katika shule za upili za umma nchini.

“Tume imeamua kusitisha usajili wa kuajiri walimu wapya kama ilivyokuwa imepanga hapo awali baada ya walimu kushiriki mgomo, lakini wale ambao tumekuwa tumewasajili na kuajiri kikandarasi wametumwa katika mashule. Tumeamua kusitisha shughuli hiyo kwa kutii agizo la mahakama,” alisema Rugut.

Rugut ameeleza kuwa tayari walimu 56 wa shule za msingi na 34 wa shule za upili kufikia siku ya Ijumma wiki iliyopita walikuwa wamesajiliwa kabla ya agizo hilo la mahakama kusistisha zoezi hilo na akasema kwamba walimu hao wametumwa katika shule mbalimbali.

“Japo tumesitisha usajili huo wa kuajiri walimu wapya katika kaunti ya Mombasa, tumetuma walimu 56 kwa shule za msingi na 34 kwa shule za upili za umma ambao tulikuwa tuwewasajili kabla ya agizo la mahakama kutolewa kwa sabubu tuko pia na uhaba wa walimu katika shule zetu,” aliongeza Rugut.

Tume ya TSC iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya walimu kudinda kurejea kazini wakidai nyongeza yao ya asilimia 50 hadi 60 huku serikali ikisema kwamba haiwezi kumudu gharama ya kuwalipa walimu.

Kwa sasa vyama vya kutetea maslahi ya walimu Knut na Kuppet pamoja na walimu wanasubiri kuona iwapo serikali itatimiza agizo la mahakama la kuwalipa walimu kwa muda wa siku 90 baada ya walimu kutii agizo la mahakama na kusitisha mgomo.