Chifu wa eneo la Kesses Sally Letting amewahikishia wanakijiji usalama wao licha ya hofu za mashambulizi ya kigaidi katika eneo hilo.
Akizungumza katika hafla ya mazishi ya mwendazake Bi Mary Birgen iliyoandaliwa Kesses siku ya Jumanne, Chifu huyo aliwataka wanakijiji wasiwe na hofu yoyote kwani tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha matendo kama hayo hayashuhudiwi katika eneo hilo.
“Ninajua kuwa kuweko kwa Chuo Kikuu cha Moi katika eneo hili limetupa hofu ya mashambulizi ya kigaidi ikikumbukwa kuwa tawi la Chuo hiki mjini Garissa lilishambuliwa. Tusiwe na hofu zozote kwa sababu kama serikali, tunafanya kila tuwezayo ili kuwapa usalama,” alielezea Bi Letting.
Chifu huyo pia alifutilia mbali madai kuwa kuna baadhi ya vijana katika eneo hilo ambao wanashukiwa kujiunga na kundi gaidi la Al Shabaab, huku akiwaomba wanakijiji wenye ujumbe kama huo au wanaoshuku wengine kuwasilisha taarifa hizo kwa polisi haraka iwezekanavyo.
“Kama serikali tuko mbioni kupigana na vita dhidi ya ugaidi hivyo tunaomba mtusaidie katika vita hivi ili tuishi kwa amani na kuzuia tendo lolote la kigaidi katika eneo hili,” alisema Letting.
Hafla hiyo ya mazishi pia ilihudhuriwa na naibu chifu wa eneo hilo pamoja na viongozi wa eneo hilo ambao pia walihakikishia wanakijiji usalama wao na kuwataka wasiwe na hofu yoyote.